KKKT kupambana na mmomonyoko wa maadili.
KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani lina lengo la kukusanya Sh milioni 220 za ununuzi wa vifaa vya kuboresha urushaji wa matangazo wa Redio Upendo FM iliyopania kupambana na mmomonyoko wa maadili katika jamii, imeelezwa.
Akizungumza wakati wa kuzindua mpango wa kuchangia redio hiyo jijini Dar es Salaam juzi, Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kilutheri Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji George Fupe alisema kanisa limedhamiria kuhakikisha usikivu wa chombo hicho cha habari unakuwa mzuri kwa ajili ya kuelimisha jamii masuala mbalimbali.
“Wakati huu nchi hii inaonesha kuwepo kuporomoka kwa maadili tofauti na miaka ya nyuma.
Tumeona mambo mengi yakijitokeza kama vile kukithiri kwa rushwa, kukosa uwajibikaji na vijana kutumbukia katika vitendo viovu. Sisi kama kanisa tumeona tujitokeze kukipa nguvu chombo hiki ili kitumike kufikisha ujumbe kwa jamii,” alisema.
Mchungaji Fupe aliwaomba waumini wa KKKT na watu wengine wenye mapenzi mema kujitoa kwa moyo kuchangia ili zipatikane Sh milioni 220 zinazohitajika kwa kuanzia kwa ajili ya kununulia vifaa vya kuboresha urushaji wa matangazo.
Aliongeza kusema kwamba licha ya mahubiri mbalimbali ya kukemea maovu ambayo yamekuwa yakifanywa na watumishi wa Mungu kwenye Ibada, kuna umuhimu mkubwa wa kutumia vyombo vya habari kama redio, magazeti na televisheni kufikisha ujumbe kwa jamii kwa kuwa ujumbe kupitia vyombo hivyo unawafikia watu wengi kwa muda mfupi.
Meneja Mkuu wa kituo hicho cha Redio cha Upendo, Agatha Lema alisema kuwa katika kuboresha usikivu kwa kuanzia, redio hiyo inahitaji kununua vifaa vya kisasa vya kurusha matangazo kwa masafa marefu na kujenga studio ya kurushia matangazo ili iwe ya kisasa kuendana na wakati wa sasa ambapo matangazo yanarushwa kwa kutumia teknolojia mpya ya mfumo wa digitali.
Alisema kuwa Upendo FM ambayo inamilikiwa na KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani mbali na kutangaza habari njema kwa watu wote pia ina vipindi vya kuelimisha jamii na kwa sasa inasikika katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Morogoro na Zanzibar.
Naye Mratibu wa maandalizi ya tamasha litakalofanyika mwanzoni mwa Mei na kuwakutanisha waimbaji wa nyimbo za Injili, Melkizedek Benjamini wa Kampuni ya PR Communication alisema maandalizi yote ya mpango huo yanaendelea vizuri ambapo wamealikwa waimbaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi akiwemo Sara K na Ruben Kigame kutoka nchini Kenya.
No comments: