Hatimaye Charles Ekelege ahukumiwa kwenda jela miaka mitatu
Aliyekuwa
Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Nchini (TBS), Charles Ekelege amehukumiwa na
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwenda jela miaka mitatu na kuilipa serikali
Dola 42,543 za Kimarekani, baada ya kupatikana na hatia ya makosa matatu
ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa asilimia 50.
Kadhalika,Ekelege anadaiwa kutoa asilimia hiyo ya punguzo la tozo ya utawala kwa
Kampuni mbili Kampuni ya Jaffar Mohamed Ali Garage na Kampuni Quality
Motors na kulisababishia shirika hilo hasara ya dola hizo.
Hukumu
hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Augustina Mmbando baada ya kupitia
ushahidi wa pande zote mbili na mahakama yake kumuona mshtakiwa bila kuacha
shaka ana hatia.
Hakimu
alisema ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ulieleza mahakama kwamba
mshtakiwa kupitia wadhifa wake alifanya maamuzi bila kinyume na sheria za TBS
zinazomwelekeza kuwasilisha masuala yote ya kiutendaji kwenye Bodi ya
Wakurugenzi.
Alisema
kitendo cha kutoa msamaha kwa kampuni hizo bila kuacha shaka moja kwa moja
mahakama imeona alitumia madaraka yake vibaya.
“Kwa
upande wa shitaka la pili, kiongozi yeyote katika Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania anapokuwa madarakani ni kwa ajili ya maslahi ya taifa,
lakini mshtakiwa alikosa uzalendo na kutumia madaraka yake vibaya kuhujumu
uchumi” alifafanua hakimu kuhusu ushahidi wa Jamhuri.
“Mahakama
inamuona mshtakiwa ana hatia katika kosa hili la pili la kujumu uchumi … pia
mshtakiwa amesababisha watanzania waliompa dhamana kukosa kula keki ya taifa
lao kwa kujinufaisha yeye binafsi” alisema hakimu huyo na kuongeza kuwa.
“Katika
ushahidi uliotolewa na mshtakiwa alikiri kufanya maamuzi bila kupata baraka na
kibali cha Bodi ya Wakurugenzi na kwamba aliidanyanya mahakama” alisema Hakimu
Mmbando.
Akifafanua
zaidi alisema mshtakiwa alidai kuwa katika kutoa maamuzi pinguzo kwa kampuni
hizo alishirikisha menejimenti na kwamba shirika lilikuwa na utaratibu wa
kufanya kikao kila siku asubuhi.
Hata
hivyo, shahidi wa pili wa utetezi Thomas Mlugulu alishindwa kuieleza mahakama
wajumbe waliokuwa wakihudhuria kikao cha cha asubuhi cha shirika kwa kila siku
zaidi ya kumtaja Betwel Matemba ambaye alishakufa na hawezi kufika mahakamani.
Alisema
ushahidi wa utetezi ulikuwa dhaifu kushindwa kukanusha ushahidi wa Jamhuri
ulioweza kuithibitishia mahakama ukweli kuhusu mashitaka yanayomkabili Ekerege.
Hakimu alisema
mahakama pia inamtia hatia mshtakiwa kwa shitaka la tatu la kuisababishia
serikali hasara ya dola hizo na kuwasababishia watanzania kukosa kula keki ya
taifa lao.
Hakimu
Mmbando alitoa nafasi kwa mawakili wa pande zote mbili kutoa hoja kabla ya kusoma
adhabu.
Mwendesha
Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Janeth
Machulya, alidai kuwa kulingana na makosa aliyotiwa hatiani mshtakiwa kwamba
alipewa dhamana na rais pamoja na watanzania lakini aameshindwa kuwa mzalendo.
“Kwa kuwa
mshtakiwa ameshindwa kuwa mzalendo kwa mamlaka aliyopewa na wananchi, tunaomba
mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa vigogo wote wanaopewa madakara
na kuyatumia vibaya,” alidai na kuongeza.
“Mheshimiwa
kwa kosa la uhujumu uchumi mahakama izingatiee utoaji wa adhabu kulingana na
sheria ya kosa hilo inavyoelekeza” alisema Machulya aliyeongoza mashahidi wa
Jamhuri katika kesi hiyo na mahakama kumtia hatiani kigogo huyo.
Wakili wa
utetezi Majura Magafu alidai kuwa mahakama imuonee huruma mshtakiwa kwa sababu
ana familia inamtegemea.
Pia,
wakili huyo alidai kuwa mshtakiwa anajutia makosa aliyofanya na kwamba
akipewa nafasi hawezi kurudia.
Hukumu
hiyo iliyoanza kusomwa saa 6:20 mchana hadi saa 8:10 hakimu aliahirisha kwa
nusu saa kabla ya kusoma adhabu.
Saa 8:49
mahakama iliyoketi chini Hakimu Mmbando ilianza shughuli zake.
Akisoma
adhabu hiyo, hakimu alisema Viongozi wote wa serikali wako juu kwa ajili ya
kulinda maslahi ya taifa ili kulinda na kuangalia nchi na mali zake, siyo
kuongoza kwa matakwa ya kiongozi husika.
“Mshtakiwa
unastahili kuhukumiwa ili kuwa mfano kwa viongozi wengine wanaochezea keki ya
taifa hili kwa manufaa yao binafsi… unakwenda jela mwaka mmoja kwa kosa la
kwanza, mwaka mmoja kwa kosa la pili na mmoja mwingine kwa kosa la tatu na
ailipe serikali fedha alizoisababisha hasara” alisema Hakimu Mmbando.
Baada ya
hukumu kusomwa;
Mshtakiwa
alianza kububujikwa na machozi huku watu wanaodaiwa kuwa familia yake wakiangua
vilio kwa sauti wakati mpendwa wao akiwa chini ya ulinzi tayari kwenda gerezani
kuanza kutumikia kifungo.
Watu
mbalimbali waliokuwa katika viunga vya mahakama hiyo walimzunguka mshtakiwa
huyo huku kila mmoja akisema lwake’jamani jela ni jela’ wengine ‘tatizo hizo
fedha alizoambiwa alipe anazo au alishakula zote’ walisikika wakizunguma.
Mapema
Mwaka 2012, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Cyril Chami aliondolewa
katika wadhifa huo kutokana na kashfa ya kutoa punguzo la tozo na baadaye Mei
21, mwaka 2012, mshtakiwa alisimamishwa kazi kama Mkurugenzi wa TBS ili kupisha
uchunguzi na hatimaye jana kuhumiwa.
Katika
kesi ya msingi, Ekelege anadaiwa kuwa kufanya matumizi mabaya ya madaraka kwa
kutoa asilimia 50 ya punguzo la tozo ya utawala kwa kampuni hizo mbili.
Pia,
ilidaiwa kuwa Machi 28, mwaka 2008 na Agosti 7, mwaka 2009, katika ofisi za TBS
zilizopo wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu Ekerege
alitumia madaraka yake vibaya.
Ilidaiwa
kuwa mshtakiwa huyo alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa punguzo la asilimia
50 ya ada ya utawala kwa kampuni hizo bila idhini ya baraza la utendaji la TBS
kinyume cha sheria namba 2 kifungu kidogo cha (3) ya TBS ya mwaka 2005.
Ilidaiwa
kuwa kitendo hicho kiliziongezea kampuni hizo faida ya Dola 42,543 za
Kimarekani sawa na (kwa wakati huo) Sh. Milioni 68,068,800.
Upande huo
wa Jamhuri ulidaiwa shitaka la pili, katika tarehe na mahali pa tukio la
kwanza, mshtakiwa alilisababishia shirika kupata hasara ya fedha hizo.
No comments: