Tuesday, February 25 2025

Header Ads

SUGU APANDISHWA TENA KIZIMBANI.



MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Mr. II Sugu jana alipandishwa kizimbani kwa mara nyingine tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi yake ambayo anatuhumiwa kufanya kusanyiko la umma kinyume cha sheria.

Sugu alipandishwa kizimbani akiwa pamoja na watuhumiwa wenzake wawili ambao ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija, maarufu kwa jina la Mzee wa Upako na Katibu mwenezi wa chama hicho wilaya ya Mbeya Mjini, Job Zebedayo Mwanyerere.

Baada ya watuhumiwa wote kusimama kizimbani, Mwendesha mashataka, Wakili wa Serikali Apimaki Mabrouk alisema ingawa upelelezi wa shauri hilo umekamilika, lakini kuna mambo ya kisheria ambayo hayajakaa sawa, na hivyo akaiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya watuhumiwa kusomewa maelezo ya awali.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya Mkoa wa Mbeya, Michael Mtaite aliiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 27, mwaka huu, siku ambayo watuhumiwa watasomewa maelezo ya awali.

Katika kesi hiyo, Sugu na wenzake wanadaiwa kuwa Julai 8, mwaka huu watuhumiwa hao wakiwa katika eneo la Nzovwe Jijini Mbeya kwa pamoja waliitisha na kufanya mkutano wa umma pasipo kutoa taarifa kwa ofisa wa Polisi wa eneo husika.

Kitendo hicho kinadaiwa kuwa ni kinyume cha kifungu cha 43 (i) na kifungu cha 46(iia) cha sheria ya Polisi kama ilivyorekebishwa mwaka 2002.

Hakimu Mteite alisema dhamana za watuhumiwa wote zinaendelea hadi hapo kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo Septemba 27, mwaka huu.

Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo umati mkubwa wa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) uliokuwa umefurika mahakamani hapo ulimzingira na kumpongezwa wakati mbunge huyo makitoka mahakamani.

Kabla ya kuondoka kwenye viwanja vya mahakama hiyo, Sugu alisalimiana na wafuasi wake waliofika mahakamani hapo kusikiliza kesi hiyo na kisha akaondoka kwenda katika kata ya Iyunga kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya wananchi wanaodai fidia baada ya Serikali kuchukua maeneo yao kwa ajili ya upanuzi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya (MIST).

No comments:

Powered by Blogger.