Askofu Kilaini na Nzigirwa Wafunguka Tuhuma Zinazowakabili
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini. |
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini amekiri kupokea
Sh80.5 milioni kutoka kwa Mkurugenzi wa VIP Engeering, James Rugemalira
akisema si mara yake kwa kwanza kupokea fedha kutoka kwa mfanyabiashara
huyo kwa kuwa mara nyingi huwa anachangia kwa uwazi miradi ya jamii.
Askofu huyo alikuwa akizungumzia Ripoti ya Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC), iliyosomwa bungeni juzi ikimtaja kuwa ni
miongoni mwa viongozi wa dini na watu wengine waliopokea mabilioni
kutoka katika akaunti ya escrow.
Mkurugenzi wa VIP Engeering, James Rugemalira. |
Katika ripoti hiyo, Zitto aliwataja viongozi wengine wa dini
walioingiziwa fedha katika Benki ya Mkombozi inayomilikiwa na Kanisa
Katoliki kuwa ni Askofu Eusebius Nzigirwa (Sh40.4 milioni) na Padri
Alphonce Twimanye Simon (Sh40.4 milioni).
Akizungumza kwa simu jana, Askofu Kilaini alisema Rugemalira
hupendelea kuchangia kwa uwazi miradi ya kijamii na si yeye peke yake
aliyempatia mchango, bali kuna watu wengine wengi ambao wameshampatia na
kazi yake ni kuipokea na kuifikisha sehemu husika.
Hata hivyo, kabla hajafafanua zaidi hoja yake, simu ilikatika na baadaye hakupatikana tena.
Hata hivyo, jana askofu huyo alinukuliwa na Gazeti la Mawio
toleo la jana akisema fedha alizozipokea kutoka kwa Rugemalira ni kwa
ajili ya miradi mbalimbali inayoendeshwa na Kanisa Katoliki.
“Ndiyo nimepokea fedha kutoka kwa James na hii siyo mara ya
kwanza, kwani mara nyingi amekuwa akichangia miradi mbalimbali ya
kijamii,” alisema Askofu Kilaini.
Alipotakiwa na gazeti hilo kuwataja wengine waliochangia kanisa
lake na kama nao wamechanga kutoka kwenye fedha za akaunti ya escrow,
alisema yeye hayumo kwenye michango hiyo.
Alipoulizwa anawezaje kusema hayumo kwenye orodha ya waliopewa
fedha kutoka akaunti ya escrow wakati anakiri kuwa aliingiziwa mamilioni
ya shilingi na Rugemalira, alisema michango inayoletwa kwake haina
siri, hivyo wezi halisi ndiyo wakamatwe.
“Michango inayoletwa kwangu haina siri, shikeni wezi halisi,” alisema.
Askofu Nzigirwa
Kwa upande wake, Askofu Nzigirwa ambaye alirithi kiti cha
Kilaini, cha Askofu Msaidizi Jimbo Kuu la Dar es Salaam ameeleza
kushtushwa kwake na ripoti ya PAC iliyomtaja yeye na Kilaini kuhusika
katika uchotwaji wa Sh306 bilioni za escrow.
Hata hivyo, kiongozi huyo alisema anaandaa taarifa itakayofafanua kwa
kina namna ambavyo fedha hizo zinazodaiwa zilitoka katika akaunti ya
escrow zilivyoingizwa katika akaunti yake pamoja na hoja na maswali
mengi yanayoulizwa na wananchi hasa waumini wa Katoliki kuhusiana na
tuhuma hizo.
“Hizo taarifa zimenishtua sana. Bado nashangaa inakuwaje mimi
naambiwa nimechota fedha kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow,”
alisema Nzigirwa alipokuwa akizungumza na gazeti hili jana.
Nzigirwa alisema anachofahamu hadi sasa fedha zilizoingizwa
katika akaunti yake hazihusiki na escrow lakini atafanya uchunguzi ili
kupata undani wa fedha hizo na majibu yote yatakuwa katika taarifa
atakayoitoa kwa vyombo vya habari siku yoyote kuanzia leo.
CDT...Mwananchi
No comments: