Uthibitisho Waziri William Lukuvi Kutaka Kuiba Ripoti ya PAC Huu Hapa.
Viongozi wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe na Deo Filikunjombe wamemtuhumu Waziri William Lukuvi kuwa alitaka kuiba ripoti ya kamati yao kuhusu uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
MWENYEKITI WA PAC BW:ZITO ZUBERI KABWE AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI |
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wabunge hao wawili kutoka Chadema na CCM walilieleza kuwa jaribio hilo lilishindikana baada ya wao na mjumbe mwalikwa, Luhanga Mpina (CCM) kuamua kukesha wakiilinda ripoti hiyo tangu ilipokuwa ikichapwa hadi ilipowasilishwa bungeni.
“Si kweli,” alisema waziri huyo wa nchi anayehusika na sera, utaratibu na Bunge.
Bunge pia lilitaka hatua za kisheria zishughulikie watu wote waliohusika kwenye sakata hilo, wakiwemo wanasiasa waliopokea fedha za mgao, taasisi za kifedha zilizohusika kufanikisha miamala haramu na wafanyabiashara waliohusika.
Vikwazo
Akizungumzia
vikwazo walivyokumbana navyo wakati wa kutekeleza majukumu yake, Filikunjombe
alisema kamati hiyo, iliyokuwa na wajumbe 24, watatu wakiwa waalikwa, kati yao
19 kutoka CCM na watano kutoka upinzani, walipata vikwazo vingi ikiwa ni pamoja
na jaribio la kurubuniwa.Filikunjombe alisema wajumbe wa PAC waliamua kuwa kitu kimoja na kuweka itikadi zao pembeni licha ya watu mbalimbali kutumia fedha kutaka kuwagawa ili wasisimamie ukweli. “Unajua sakata la Escrow linawagusa watu wenye fedha ambao walianza kuuaminisha umma kuwa wajumbe wa PAC na sisi tumekula fedha hizo. CCM ilitakiwa kuuchukulia wizi huu kama ajenda yake kuu,” alisema.
Alisema hakupendezwa na ushauri uliotolewa na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge kuhusu adhabu wanazotakiwa kupewa watuhumiwa wa wizi wa fedha hizo,
wakati na yeye akiwa miongoni mwa watuhumiwa kutokana na kudaiwa kupewa Sh1.6 bilioni. Kuhusu suala la watuhumiwa kujiuzulu, Filikunjombe alisema siku zote Serikali haipendi kusimamiwa na Bunge, bali inapenda kushauriwa na kwamba hiyo ndiyo sababu ya Serikali kukataa pendekezo la PAC la wahusika kujiuzulu bila kuziomba mamlaka za uteuzi kutekeleza hilo.
“Ukitizama suala la (mkataba wa ufuaji umeme) Richmond si kama fedha zilichotwa wazi, lakini hili la escrow fedha zimechotwa na waliochota wanajulikana, sasa iweje tushikwe na kigugumizi kutaka wajiuzulu. Tena fedha hizo ni mara tatu ya zile za Richmond,” alisema.
Zitto ataja
vitisho
Kwa upande wake
Zitto alisema: “Vitisho vilikuwa vingi, lakini siyo kutoka serikalini bali
kutoka kwa watu binafsi ambao wanahusika na uchotwaji huu wa fedha.
“Mfano kupigiwa
simu kuambiwa niachane na jambo hili ama sivyo nitakufa au hata kutishiwa
kuchafuliwa. Vipeperushi vya matusi dhidi yangu vilisambazwa kwenye nyumba za
wabunge ili
kuniondolea heshima na uhalali wa kuongoza vikao.”
Akieleza sababu
za kuilinda ripoti, Zitto alisema: “Kwa sababu Serikali ilikuwa inataka kuipata
mapema ili kuichakachua, hatukulala siku hiyo mpaka taarifa yetu ilipokuwa
taarifa rasmi ya Bunge. Mimi, Deo na Luhaga ndio tuliopewa jukumu hilo.”
Alisema hawakupata usumbufu kutoka
serikalini, isipokuwa pale zilipoanza kujengwa hoja kuwa mahakama imezuia
mjadala.
Alipoulizwa
kama watuhumiwa wa sakata hilo waliwahi kumfuata kwa namna yoyote ile alisema:
“(Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen) Masele peke yake ndiye alikuwa
akiomba msaada. Maswi alinipigia simu siku moja tu kuomba msaada, lakini
sikumjibu kitu. PAC tunaamini kuwa tumetenda haki kwa wananchi.”
Maswi
alipopigiwa simu jana alipokea na mwandishi alipojitambulisha, alikata simu na
alipopigiwa tena kwa simu tofauti alipokea na alipoulizwa swali hilo aliikata
tena simu. Ripoti ya PAC ilisomwa na kujadiliwa bungeni na kusababisha
mtikisiko mkubwa kutokana na mapendekezo yake kuwagusa watu wazito ndani ya
Serikali.
Mapendekezo
hayo yanataka Mwambalaswa, Ngeleja na Chenge wavuliwe nyadhifa zao, sambamba na
wote waliohusika katika muamala wa Akaunti ya Escrow kuchukuliwa hatua baada ya
uchunguzi.
CDT...Mwananchi
No comments: