Waziri Mwakyembe azindua magari ya milioni 840/- JNIA
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe leo
amezindua magari 54 ya abiria ya Chama cha Ushirika cha Madereva wa Taksi
katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Jijini Dar es
Salaam yenye thamani ya sh. Milioni 840 kuboresha usafiri wa abiria.
Hafla hiyo ya uzinduzi imefanyika katika eneo la
kiwanja cha zamani cha Ndege, Terminal I, makao makuu ya Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Tanzania (TAA) ambapo ameiagiza TAA kuhakikisha inaipa hadhi JNIA kama
alivyokuwa mwenye jina hilo, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“TAA hakikisheni JNIA inabeba jina la Julius Nyerere
kwa mandhari, utendaji na vyombo vya usafiri, “ Waziri Mwakyembe amemweleza
Mkurugenzi wa JNIA, Bw. Moses Malaki na uongozi wa TAA kwa jumla.
Waziri Mwakyembe amesema, hatua ya ATACOS kununua
magari hayo inaongeza ubora wa huduma na hadhi ya kiwanja cha ndege cha JNIA na
kwamba magari hayo yatasaidia kuchukua hata wageni wa Serikali
Alisema mradi huo wa magari ni mkubwa kwa wana
ushirika hao na magari yao ni ya viwango vya juu na hata kwa mbali ukiyaangalia
magari hayo, yana viwango vikubwa na Serikali ikipata wageni zaidi ya 500 kwa
mpigo, haitahangika kutafuta magari kwani hayo yapo. Thamani ya gari moja ni
sh. Milioni 15 na ni mkopo wa Equity Bank.
Hata hivyo, Waziri Mwakyembe amewataka madereva hao
kuzingatia usafi wa magari na wao wenyewe kwani wageni wakikodi magari hayo na
kuyakuta ni nadhifu na wao ni wasafi, ndio kielelezo cha nchi yetu.
“Naheshimu sana kazi mnayofanya. Ina add value
(ongeza thamani), “ waziri Mwakyembe amesema na kuutaka uongozi wa TAA utambue
mchango wa madereva hao kwani magari yao ni mazuri na hata katika jengo la tatu
la abiria (TB III) linalojengwa, yanaweza kupewa fursa.
Amewataka kuyatunza kwa kuyavika vita vyeupe na wao
kuvaa sare nyeupe na kusimamia viwango kwa kuwa na zaidi ya sare moja nyeupe
ili hata akiingia mtalii, ajue kuwa anaingia nchi ya wastarabu.
Hata hivyo, Waziri Mwakyembe ameeleza kusikitishwa
na madereva hao kuushitaki uongozi wa TAA mahakamani kuhusu haki ya kuendesha
biashara ya taksi JNIA. Amewaeleza asingeweza kuwasaidia kutatua kero hiyo kwa
kuwa kuna kesi hiyo bado iko mahakamani hadi leo.
“Sijui nani aliwashauri. Mimi ni Kiongozi wa
Serikali tena ni Wakili wa Mahakama Kuu. Siwezi kuingilia utendaji wa mhimili
mwingine wa chombo cha haki. Nitaonekana wa ajabu. Mikono yangu imefungwa
katika hili, “ aliwaeleza na kuacha kujibu kero zao kuhusu mgogoro huo.
Katika risala yao kwa Waziri Mwakyembe, Katibu wa
stendi ya madereva teksi JNIA, Mohammed Mashombo amemweleza Waziri mafanikio na
kero zao tangu waanze 2000 na kuomba awasaidie.
Hata hivyo, uongozi wa TAA ulimweleza Waziri
Mwakyembe awali kuwa, madereva hao waliushitaki kuhusiana na mkataba wa kufanya
biashara JNIA na kesi hiyo inaendelea hadi leo na kwamba mengi ya madai
waliyomtaka awasaidie, ndio wameyewasilisha mahakamani.
Hafla hiyo imehudhuriwa na wageni mbalimbali na
watendaji wa TAA, Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege Tanzania, Mrajisi wa
Vyama vya Ushirika, Meneja wa TRA Mkoa wa Temeke, Mkurugenzi wa Equity Bank,
Mkurugenzi wa ABG na Afisa Biashara wa Manispaa Temeke.
Imetolewa na Godfrey John Lutego
Afisa Uhusiano – Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (TAA)
No comments: